SEDUCE ME ILIVYONOGA NA BAISKELI ZA ROSTAM FIESTA MWANZA – Bingwa | Bingwa
NA MWANDISHI WETU
WIMBO wa Seduce Me wa mkali wa Bongo Fleva, Ali Kiba, ameendelea kubamba katika maeneo mbalimbali, wikiendi iliyopita ukiwachizisha vilivyo wakazi wa Mwanza waliohudhuria tamasha la Tigo Fiesta 2017, kwenye Uwanja wa CCM Kirumba.
Lakini pia, uhondo wa wimbo huo ulinogeshwa zaidi na wakali wa hip hop, Roma Mkatoliki na Stamina, wanaounda umoja walioupa jina la Rostam, ambao walipanda jukwaani kivingine kwa kila mmoja kuwa na baiskeli yake na kuweka kitu tofauti kwenye wimbo wao wa Huku Ama Kule.
Manjonjo hayo yaliyofanywa na Rostam pamoja na uhondo wa Seduce Me, uliufanya Uwanja wa CCM Kirumba kulipuka kwa shangwe kutoka kwa mashabiki wa burudani waliofika uwanjani hapo kupata burudani kutoka kwa sanii wao wakali wa hapa nchini.
Kampuni ya Simu za mkononi ya Tigo Tanzania, alikuwa ni msanii wa kufokafoka, Rosa Ree, ambaye alifungua pazia la burudani na kuonyesha jinsi gani anakuja kwa kasi katika muziki pale alipoimba kwa umahiri wa hali ya juu nyimbo zake, zikiwamo Mchaga Mchaga na Up In The Air.
Baada ya msanii huyo, alifuatia mwanadada Lulu Diva, ambaye naye alikonga nyoyo za mashabiki kama ilivyokuwa kwa sanii wengi waliopata nafasi ya kufanya yao siku hiyo, Ommy Dimpoz, Rayvanny, Fid Q, Joh Makini, Ben Pol, Nandy, Jux, Maua, Weusi, Aslay, Young Killer, Darasa, Bill Nas, Future JNL, Bright, Eduboy na wengineo.
Kwa ujumla, tamasha hilo lilifana vilivyo jijini Mwanza, ambapo mashabiki lukuki walihudhuria kuonyesha jinsi Watanzania wanavyopenda burudani, lakini pia wasanii wao.
Akizungumzia tamasha hilo, Meneja wa Tigo Kanda ya Ziwa, Edgar Mapande, alisema mwaka huu wameamua kudhamini ili kusaidia vipaji vya wasanii na kuwaletea wateja wao burudani, kadhalika kuwapatia vifurushi mara wanunuapo tiketi za Tigo Fiesta kwa Tigopesa.
“Mteja wetu akinunua tiketi kwa Tigopesa, anapata Mbs 100, dakika 100 na sms 100 bure,” alisema Mapande na kuongeza kuwa, tamasha hilo litaendelea Ijumaa hii mkoani Tabora kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi.
The post SEDUCE ME ILIVYONOGA NA BAISKELI ZA ROSTAM FIESTA MWANZA appeared first on Bingwa.
from Habari Za Tanzania
via Read More
Comments